skip to Main Content

Je Nini Maana ya shule salama kwa watoto?

Hakika miaka miwili hii ya 2018/2019 imekuwa miaka ya matukio mengi sana ya ukatili dhidi ya watoto. Tumeshuhudia mauaji makubwa ya watoto kule Mkoani Njombe lakini lakushangaza zaidi ni tukio la MWANAFUNZI wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibeta iliyoko Manispaa ya Bukoba, Sperius Eradius (13), aliyefariki dunia kwa kipigwa na mwalimu wake akituhumiwa kuiba pochi ya mwalimu. Kama watetezi wa haki za watoto tunajiuliza hata sehemu ambayo ingepaswa kuwa salama kabisa ndipo ambapo watoto wanapoteza maisha kwa sababu ya vipigo kutoka kwa walimu?.

Makala hii inaleta uchambuzi hasa katika kujenga mazingira ya shule salama kwa watoto ambayo yatamfanya mtoto kujisikia huru na salama katika kufikia malengo yake ya elimu.

Elimu ni haki ya msingi ya mtoto na mtanzania yeyote. Lakini mazingira salama kwa watoto wanapokua mashuleni bado imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kufikia malengo ya haki ya elimu kwa watoto. Watoto wanakumbana na adhabu za vipigo, ukatili wa kingono na hata udhalilishwaji wakiwa mashuleni.

Adhabu za vipigo mashuleni ni moja ya sababu ambazo zinafanya mazingira ya shuleni kutokua salama kwa watoto. Mnamo mwezi Novemba, 2018 serikali kupitia Naibu Waziri wa Elimu Mh.William Ole Nasha (MB) ilipiga marufuku Walimu kutoa adhabu ya viboko kwa mwanafunzi bila kibali maalum na pia ilipiga marufuku Walimu kutembea na viboko, Mh.Ole Nasha (MB) alitoa agizo hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum CCM Rose Tweve aliyetaka kujua kauli ya Serikali kwa Walimu wanaokiuka sheria za adhabu kwa Wanafunzi. Licha ya serikali kupiga marufuku adhabu za viboko mashuleni bado hakuna miongozo yoyote iliyotolewa na serikali juu ya usimamizi wa nidhamu mashuleni na watoto wanaendelea kupigwa na kuumizwa.

Adhabu za viboko mashuleni kwa tafiti nyingi zinaonesha ni kwa sababu ya msongo wa mawazo kwa walimu na pia kukosa mbinu mbadala za kusimamia nidhamu kwa wanafunzi na kuamini kwamba adhabu kali za viboko ndio njia pekee inayoweza kusimamia nidhamu ya shule.

Utafiti uliofanywa na HakiElimu kwa kuuliza swali “Shule Salama ni nini”? ambapo takribani watu 6,000 walishiriki wengi wao waliongelea shule salama kama ni madarasa mazuri, mpangilio, usafi, walimu, vitabu,  na vyoo. Wachache sana waliongelea mazingira ambayo walimu hawakupigi. Hii inaonesha taswira ya jinsi gani hata jamii iko nyuma juu ya athari za adhabu zilizopitiliza mashuleni.

SHERIA ZA TANZANIA JUU YA ADHABU YA VIBOKO MASHULENI

Sheria inayosimamia maswala ya elimu Tanzania ni Sheria ya Taifa ya elimu (National Educations Act, 1978). Sheria hii ndani ya kifungu cha 60 (1) (O) kinampa waziri mwenye dhamana kutengeneza kanuni ambazo zitaratibu na kusimamia utoaji ya adhabu za viboko mashuleni. Hivyo kanuni za uratibu na usimamizi wa utoaji wa adhabu mashuleni (The National Education (Corporal Punishment) Regulations, 1979 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2000 kupunguza idadi ya viboko kutoka 6 hadi viboko 4, inatoa maana ya adhabu ya viboko mashuleni na jinsi gani ya kutoa adhabu hiyo. Kulingana na kanuni hizi Adhabu ya viboko mashuleni ni adhabu inayotolewa kwa kuchapwa fimbo mwanafunzi mkononi au matakoni akiwa amevaa sare ya shule. Na pia kanuni zinaeleza kuwa adhabu hiyo itolewe na fimbo nyembamba na ambayo ni rahisi kutumika. Mwanafunzi asichapwe na kitu kingine chochote zaidi ya fimbo na asichapwe sehemu nyingine yoyote ya mwili zaidi ya zilizotajwa kwenye sheria

Kanuni hizo pia zinatoa masharti kwamba adhabu hiyo itatolewa kwa makosa makubwa ya uvunjifu wa nidhamu ya shule ambayo yatapelekea shule kuingia katika migogoro, iwe mwanafunzi amefanya nje au ndani ya shule. Pia kanuni zinasema azabu hizo ziwe za busara kwa kuzingatia ukubwa wa kosa lenyewe, umri wa mtoto, jinsia ya mtoto, afya ya mtoto, na zisizidi fimbo 4.

Licha ya kuwa hata na sheria hii ambayo ingepaswa kuondolewa kabisa bado watoto wamekua wakipata adhabu kubwa zaidi zikiwemo za kupigwa mateke, ngumi, makofi na hata kupigwa kwa kutumia vitu kama rula, vipande vya kuni au kupewa adhabu za kusimama juani kwa takribani nusu siku.

Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 (The law of the Child Act, 2009) kifungu cha 13 kinakataza vitendo vyote ambavyo vitamsababishia mtoto mateso, ukatili, matendo ya kinyama au kumdhalilisha. Lakini sheria hiyo hiyo kifungu cha 13(2) kinaruhusu adhabu ambazo zinauhalali na haijatoa mipaka ya adhabu ya viboko.

Hata hivyo serikali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto Tanzania 2017/18 – 2021/22 Mpango kazi huo una maeneo Nane ya utekelezaji. Eneo la 7 la utekelezaji ni Mazingira Salama Shuleni na Stadi za maisha. Katika eneo hili serikali ina matarajio mpaka kufika mwaka 2022 Kuondoa aina zote za ukatili katika mifumo rasmi na isiyo rasmi ya kielimu ili kuwezesha watoto na vijana (ikiwemo watoto wenye ulemavu)  kufikia malengo yao.

Hivyo kuna nia ya kuondoa ukatili huu wa adhabu za viboko kwa watoto lakini bado adhabu za viboko mashuleni inaruhusiwa kisheria kwa wasichana na wavulana licha ya matamko mbali mbali ya Serikali juu ya adhabu hizo. Kuna umuhimu wa sheria hizi pamoja na kanuni zake kupitiwa upya na kuondoa kabisa adhabu za viboko mashuleni.

NINI KIFANYIKE KUTENGENEZA MAZINGIRA SALAMA SHULENI?

Ili kutengeneza mazingira salama Shuleni ni muhimu muendelezo wa hatua kuchukuliwa na Serikali pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo zikiwemo Asasi za kiraia pamoja na Jamii kwa ujumla.

Elimu na uelewa juu ya sheria zilizopo juu ya kutoa adhabu kwa watoto ni hatua muhimu ambayo inaweza kusaidia kutengeneza mazingira salama kwa watoto mashuleni. Ikiwa ni pamoja na kuhusishwa katika upatikanaji wa sera na sheria za kuwezesha mtoto kusoma katika mazingira salama.

Ni muhimu pia serikali pamoja na kupiga marufuku adhabu za viboko mashuleni kuja na miongozo ya njia mbadala za kusimamia nidhamu mashuleni ili kuepusha dhana ya walimu kutokua na njia mbadala za kusimamia nidhamu.

Ni wajibu wa serikali Pamoja na wadau wa maendeleo, Kupitia sheria na sera kubaini mapungufu yaliyopo na kufuatilia utekelezaji wa sheria na sera. Hii ihusishe pia kutumia uzoefu na mafunzo  kutoka katika nchi mbali mbali pamoja na shule za ndani ambazo zimeweza kuondoa adhabu mashuleni.

Kujenga uhusiano mzuri kati ya mwalimu na mwanafunzi ni nguzo muhimu sana katika kufikia matarajio ya kuwa na shule salama. Elimu ya uhusiano wa mwalimu na mwanafunzi itasaidia mwalimu kutumia mbinu mbadala za kukuza nidhamu na mwanafunzi kuwa huru kuuliza na kusoma.

Wakati tunajaribu kutengeneza mazingira salama mashuleni tukumbuke pia kuihusisha jamii, walezi na wazazi ili wote tuongee lugha moja. Kama tutajaribu kuwaelewesha na kuelimisha walimu tu juu ya njia mbadala za kusimamia nidhamu za watoto wetu mashuleni na huku nyumbani kuna ukatili uliopitiliza, baba anakunywa na kupiga mama mbele ya watoto, kuna mafarakano ndani ya familia, juhudi zetu hazitafanikiwa.

Mwisho.  

Imeandaliwa na : Working Group Two(WG2) Kikosi kazi katika mradi wa Data Driven Advocacy(DDA) chini ya uratibu wa

Women in Law and Development in Africa (WiLDAF) wakishirikiana na :-

 1. Tanzania Gender Networking Program(TGNP)
 2. Tanzania Media Women Association(TAMWA)
 3. Tanzania Child Rights Forum (TCRF)
 4. Tanzania Domestic Workers Coalition(TDWC)
 5. Mwanza Youth and Children Network(MYCN)
 6. Tanzania Early Childhood Development Network(TECDEN)
 7. Zanzibar Women Lawyers Association (ZAFELA)
 8. Tanzania Association for children Advancement(ZACA)
 9. Tanzania Women Lawyers Association (TAWLA)
 10. Women Legal Aid Centre(WLAC)
 11. Women with Disability Network
 12. Mulika Tanzania
 13. Tanzania Youth Partnership country wide(TYPC)
 14. Haki za Wanawake (HAWA)
 15. Community Focus on Teenage and single mothers welfare(CFTSW)
 16. Vijana Assembly.
 17. People Development Forum (PDF)

 

 

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Back To Top