skip to Main Content

Azimio La Viongozi Wa Dini

Azimio La Viongozi Wa Dini Katika Kuhamasisha Ushiriki Wa Wanawake Katika Uongozi Na Ngazi Za Maamuzi

Sisi Viongozi wa Dini tuliokutana leo tarehe 15/10/2020 Jijini Dodoma, katika mdahalo juu ya “Nafasi ya Viongozi wa Dini Kuhamasisha Ushiriki wa Wanawake katika Uongozi na Ngazi za Maamuzi”;

Kwa kutambua nafasi ya mwanamke katika jamii na hata kidini kama ilivyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu;

Na, kwa kutambua ushiriki hafifu wa wanawake katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi ijapokuwa takwimu zinaonyesha idadi ya wanawake ni zaidi ya 51% ya idadi ya watu (kwa mujibu wa sensa ya idadi ya watu na makazi,2012)

Na, kwa kutambua changamoto mbalimbali zinazopelekea ushiriki hafifu wa wanawake katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi ikiwemo, mfumo dume, mila na mitizamo hasi, rushwa katika vyama vya siasa, utayari katika vyama vya siasa pamoja na ukatili  na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake kwenye majukwa ya kisiasa,

Na, kwa kutambua nafasi yetu kama viongozi wenye ushawishi ndani ya jamii kwa kauli moja tumeazimia kutoa azimio hili ili kushawishi Serikali na kuhamasisha jamii umuhimu wa wanawake kushiriki katika uongozi na ngazi za maamuzi.

Hali Halisi

  • Kuanzia mwaka 1985 hadi 2015 ushiriki wa wanawake Bungeni umekuwa kama ifuatavyo;
    • 1985 Wanawake walikuwa 9% ya idadi ya wabunge wote
    • 1995 Wanawake walikuwa 17% ya idadi ya wabunge wote
    • 2000 Wanawake walikuwa 21% ya idadi ya wabunge wote
    • 2005 Wanawake walikuwa 31% ya idadi ya wabunge wote
    • 2010 Wanawake walikuwa 36% ya idadi ya wabunge wote
    • 2015 Wanawake walikuwa 36.9% ya idadi ya wabunge wote
  • Kwa takwimu hizi kutoka mwaka 2010 hadi mwaka 2015 kuna ongezeko la asilimia 0.9 tu ya wanawake waliongia Bungeni, licha ya jitihada mbalimbali za serikali na wadau ikiwemo kuboresha sheria wezeshi na kutoa elimu kwa wadau na jamii kwa ujumla juu ya nafasi ya mwanamke kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo uongozi
  • Kwa upande wa Serikali za Mitaa, mwaka 2014 Jumla ya Wanawake 223 walishinda katika Nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji sawa na asilimia 1.8 ya nafasi zote, Wenyeviti wa Mitaa 435 sawa na asilimia 11 ya nafsi zilizogombewa na Wenyeviti wa Vitongoji 3,482 sawa na asilimia 5 ya nafasi zilziogombewa.
  • Katika Mwaka 2019 Wenyeviti wa Vijiji  wanawake waliopita bila kupingwa ni 246 sawa na asilimia 2.1 ya Nafasi zote za Wenyeviti wa Vijiji waliopita bila kupingwa, Wenyeviti wa Mitaa wanawake 528 sawa na asilimia 12.6 ya Wenyeviti wa Mitaa walipita bila kupingwa na Wenyeviti wa Vitongoji wanawake 4,171 sawa na asilimia 6.7 ya Wenyeviti wa Vitongoji walipita bila kupingwa.
  • Aidha, Wanawake walioshinda kwa kupigiwa kura katika nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji ni 5, Mwenyekiti wa Mtaa ni 13 na Mwenyekiti wa Kitongoji ni 96. Hivyo, jumla ya Viongozi Wanawake waliochaguliwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 ni Wenyekiti wa Vijiji 251, Mitaa 541 na Wenyeviti wa Vitongoji ni 4,267.
  • Takwimu hizi zinaonesha ongezeko dogo la ushiriki wa wanawake katika siasa na nafasi za uongozi  kwa serikali za mitaa mwaka 2019 ukilinganisha na mwaka 2014.

Nini Kifanyike

  • Viongozi wa Dini, Serikali na wadau kuendelea kuhamasisha jamii juu ya umuhimu na haki wa wanawake kushiriki katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kiuongozi
  • Viongozi wa dini kuendelea kukemea na kuzuia migogoro mbalimbali hasa lugha za kashfa dhidi ya wanawake katika majukwa ya kisiasa
  • Kuhimiza wanawake waliopo kwenye nafasi kutetea na kupaza sauti juu ya haki za wanawake katika kushiriki kwenye siasa
  • Kutoa tafsiri sahihi za vitabu vitakatifu juu ya nafasi ya mwanamke katika jamii
  • Kuandaa programu mbali mbali zinazoshirikisha wanaume na wavulana katika mchakato huu kuhakikisha usawa wa kijinsia katika maswala ya uongozi, hii itatusaidia kutomuacha yeyote nyuma.
  • Kuendelea kuwajengea uwezo wanawake kuanzia ngazi ya familia juu ya nafasi na uwezo wao mkubwa
  • Viongozi wa dini kiuandaa mitaala ya kidini inayowezesha na kuhamasisha wanawake na mabinti kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Maazimio

Viongozi wa dini tumeazimia kuwa na ajenda ya kudumu ya kutetea wanawake na kutumia majukwaa na nafasi tulizo nazo kuendelea kuhamasisha jamii juu ya ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi kuanzia kwenye taasisi tunazoziongoza mpaka ngazi za kitaifa. Hii ni kwa kuzingatia kwamba hakuna maandiko yaliyoletwa kukandamiza jinsia fulani.

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Back To Top