skip to Main Content

Je ni muhimu kuandika Wosia?

WOSIA

Wosia ni kauli inayotolewa na mtu wakati wa uhai wake kwa hiari yake kuonyesha jinsi gani angependa mali yake igawanywe baada ya kufa kwake.

Aina za Wosia

Wosia unaweza kuwa wa namna mbili;

 1. Wosia wa maandishi (ulioandikwa)
 2. Wosia wa mdomo (usio wa maandishi)

Wosia wa Maandishi                 

Wosia wa maandishi ni lazima;

 • Uandikwe kwa kalamu ya wino na sio kalamu ya risasi (inayoweza kufutwa futwa).
 • Anayetoa wosia (Muusia) awe na akili timamu.
 • Utaje tarehe ulipoandikwa (Tarehe ya wosia)
 • Utaje kuwa muusia anayo akili timamu na anausia kwa hiari yake mwenyewe.
 • Ushuhudiwe na mashaidi wanaojua kusoma na kuandika angalau wawili (mmoja wa ukoo na mwingine mtu baki), kama muusia anajua kusoma na kuandika.
 • Ushuhudiwe na mashahidi wasiopungua wane (wawili wa ukoo na wawili watu baki), kama muusia hajui kusoma na kuandika.
 • Wanaotarajia kurithi hawaruhusiwi kushuhudia wosia huo.
 • Usainiwe na muusia mbele ya mashahidi wake wakiona, kutia sahihi yake au kama hajui kusoma, aweke alama ya dole gumba la kulia.
 • Wosia unatakiwa kutiwa sahihi za mashahidi.
 • Mashahidi wanatakiwa wawe wamechaguliwa na muusia mwenyewe.

Wosia wa maandishi waweza kubadilishwa kwa wosia mwingine wa maandishi unaotaja kubadilisha wosia wa kwanza na unaofuata hatua zilezile kama ilivyoainishwa hapo juu.

Wosia wa Mdomo

Wosia wa mdomo lazima;

 • Ushuhudiwe na mashahidi wanne (wawili wa ukoo na wawili watu baki).
 • Muusia awe na akili timamu.
 • Kama mashahidi watakufa kabla ya muusia kufa, basi wosia hautakubalika na urithi utagawanywa kadri ya mpango wa urithi usio wa wosia. Mwenyewe kama anataka kuusia mali zake, atoe wosia mpya.
 • Mashahidi wawe wamechaguliwa na muusia mwenyewe.

Sheria inaweka bayana kwamba kuandikisha wosia sio lazima, bali ni hiari ya muusia. Pia wosia wa mdomo hauwezi kufuta au kubadilisha wosia wa maandishi, lakini wosia wa maandishi waweza kufuta au kubadilisha wosia wa mdomo ikiwa waliokuwa mashahidi wa wosia wa mdomo watashiriki.

Wosia waweza kubatilishwa ikiwa itathibitika kwamba muusia amepungukiwa akili kwa sababu ya wazimu, ugonjwa, ulevi au hasira ya gafla. Ni muhimu kukumbuka kwamba ni wahusika tu (warithi), wanaoruhusiwa kupinga wosia kwa sababu zilizotajwa hapo juu.

Jinsi ya Kurithithisha Wosia

Kulingana na Sheria ya Usimamizi wa Haki na Matumizi ya Sheria mbali mbali mbali, Sura  ya 358, muusia anaweza kuusia mali yake yote bila kutaja kila kitu alichonacho wakati wa kufa kwake. Ikiwa muusia anapenda kuusia sehemu tu ya mali yake, basi sehemu iliyobaki itagawanywa kulingana na masharti ya urithi usio wa wosia.

Faida za wosia

Wosia una faida zifuatazo;

 1. Muusia anapata fursa ya kufanya mgawo wa mali yake kwa kadri anavyotaka kabla ya kufariki.
 2. Muusia anapata fursa ya kuamua ni nani awe msimamizi wa mirathi yake.
 3. Wosia huepusha ugomvi wa wanafamilia na kuimarisha Amani miongoni mwa warithi na wanandugu halali.
 4. Wosia ni chombo cha kuhakikisha kwamba urithi unakwenda kwa watu ambao marehemu aliwaridhia.

Zingatio: Wosia ugusie mali za marehemu tu. Wosia ambao unarithisha mali zisizokuwa za marehemu au ambazo zilikuwa zinamilikiwa na marehemu pamoja na mtu mwingine kwa namna ya maslahi yasiyogawanyika wosia huo hautakuwa halali.

Mahali za kuhifadhi wosia

Wosia waweza kutunzwa mahali popote palipo na usalama na ulinzi wa kutosha, ili kuepuka kughushiwa. Watu wengi huchagua kutunza katika sehemu zifuatazo;

 1. Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu (RITA/WAUU).
 2. Kwenye vyombo vya kutoa msaada wa kisheria.
 3. Asasi za kidini kama kanisa au msikiti.
 4. Katika Kampuni ya uwakili.
 5. Kwa mtu yeyote asiye mrithi katika wosia husika na ana sifa za kutunza siri.
 6. Benki
 7. Mahakamani.

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Back To Top