skip to Main Content

Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati – Hotuba ya Mgeni Rasmi Waziri Dkt. Dorothy Gwajima

HOTUBA YA DKT. DOROTHY GWAJIMA (MB), WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM; MGENI RASMI MHESHIMIWA KWENYE UZINDUZI WA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA,

VIWANJA VYA LEADERS,

JIJINI DAR ES SALAAM, TAREHE 25 NOVEMBA 2022.

 • Amos Makala, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam,
 • Wakili Amon Mpanju, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, ,
 • Godwin Gondwe, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni;
 • SACP Jumanne Muliro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
 • Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Dkt. Monica Mhoja,
 • Mheshimiwa Mette Nørgaard Dissing-Spandet, Balozi wa Denmark,
 • Mheshimiwa Mary O’Neill, Balozi wa Ireland,
 • Mheshimiwa Tereza Zitting, Balozi wa Finland,
 • Mheshimiwa Peter Huyghebaert, Balozi wa Belgium,
 • Mheshimiwa Didier Chassot, Balozi wa Switzerland,
 • Ndugu Zlatan Milišić, Mratibu Mkaazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania,
 • Ndugu Manfredo Fanti, Balozi wa Jumuiya ya Nchi za Ulaya Nchini Tanzania,
 • Ndugu Hodan Addou, Mwakilishi Mkaazi wa kitengo cha Wanawake cha Umoja wa Mataifa (UN-Women),
 • Ndugu Mark Bryan Schreiner, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA),
 • Ndugu Lulu Ng’wanakilala, Mkurugenzi wa Taasisi ya Huduma za Sheria (LSF);
 • Wawakilishi kutoka Balozi na Mashirika ya Kimataifa nchini;
 • Viongozi na Watendaji Wakuu wa Idara na Taasisi za Serikali mliopo hapa;
 • Viongozi wa Dini
 • Wakuu wa Taasisi Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi mliopo;
 • Wawakilishi kutoka vyama vyote vya siasa;
 • Wawakilishi kutoka Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia wakiwemo MKUKI, SUMAUJATA;
 • Waandishi wa Habari;
 • Wageni Waalikwa;
 • Mabibi na Mabwana.

Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

Ndugu Wananchi, Namshukuru Mungu kutujaalia afya na uzima na kutuwezesha kuhudhuria Uzinduzi huu wa Kampeni ya Siku 16 za kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka huu 2022. Natoa shukrani za dhati kwa heshima kubwa ya kunialika kuwa Mgeni Rasmi kwenye Uzinduzi wa kampeni hii. Naushukuru Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Mhe Amos Makala, Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kuwa mwenyeji  wa uzinduzi wa Kampeni hii. Kwa nafasi ya pekee, nawapongeza  Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Tawi la Tanzania, Mtandao wa Mashirika yanayoshughulika na kutokomeza Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) na wadau wote kwa kuratibu vyema maandalizi ya uzinduzi huu ambao umefana sana, HONGERENI SANA.

Ndugu Wananchi, Nimejulishwa kuwa, washiriki kwenye uzinduzi huu wa Kampeni hii wametoka sehemu mbalimbali hapa nchini wakiwemo Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Dini, wanaharakati wa Haki za binadamu, Wafanyakazi, Wanafunzi na Wananchi kwa ujumla wao. Ninayo furaha kujumuika nanyi kwani uzinduzi huu kwani, pamoja na mambo mengine utanipa fursa ya kujifunza na kubadilishana mawazo juu ya mbinu za kutokomeza ukatili wa kijinsia na hivyo kuwa na jamii salama na yenye usawa kwa ustawi na maslahi mapana ya Taifa letu.

Ndugu Wananchi, kwa heshima napenda kutoa salaam za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwamba, anawatakia maadhimisho mema ya Kampeni hii muhimu ambayo itachochea kuleta mabadiliko ya fikra kuelekea kwenye jamii yenye maendeleo ya usawa wa kijinsia. Anamshukuru kila mmoja aliyeshiriki na atakayeshiriki kwenye siku hizi 16 za Kampeni hii muhimu.

Ndugu Wananchi, baada ya salaam hizo naomba kuangazia takwimu chache; Kama ilivyo kwa Mataifa mengine Duniani, Tanzania ni miongoni mwa Nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo la ukatili wa kijinsia. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2015/2016 kupitia Taarifa ya Idadi ya Watu na Afya inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 – 49 wamefanyiwa ukatili wa kupigwa au kingono katika kipindi cha maisha yao.  Kadhalika, asilimia 22 ya wanawake wenye umri huo walifanyiwa vitendo vya kingono kinyume na matakwa yao. Kwa ujumla taarifa hiyo, inaonesha hakuna tofauti kubwa ya mabadiliko katika jamii zetu kuhusu mitazamo na matendo ya jamii zetu kuhusiana na Ukatili wa Kijinsia. Hivyo, Ni dhahiri kuwa bado tuna kazi kubwa ya kuhamasisha na kuelimisha jamii zetu kubadili fikra na mitazamo inayochochea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia

Ndugu Wananchi, Kauli mbiu ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka huu ni Kila Uhai Unathamani! Tokomeza Mauaji Na Ukatili Dhidi Ya Wanawake Na Watoto. Kauli mbiu hii inatukumbusha wajibu wetu wa kuchukua hatua kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia ili kuokoa Maisha ya wanawake na Watoto. Aidha, siku za karibuni kumekuwapo na kushamiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kwenye mitandao.

Hali hii inazorotesha jitihada za wanawake za kushiriki kujiletea maendeleo. Hivyo, tuungane kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani madhara yake ni makubwa endapo jamii haitachukua hatua kukomesha au kuzuia vitendo hivi visitokee. Na tunapoungana, tubuni na tukubali mbinu mpya za kuwasilisha elimu na uhamasishaji kwa kuvunja ukimya kwani ni katika ukimya wa baadhi yetu ndiyo sehemu ya jamii hasa watoto fahamu zao zinakuwa hazielewi kuwa hicho wanachotaka kufanyiwa ni kitu kibaya au kinawapeleka kwenye ukatili mbaya.

 

Ndugu Wananchi, mtakumbuka kuwa wakati wa uzinduzi wa Kampeni hii kwa mwaka 2021, Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maagizo kadhaa kwa Wizara yangu ikiwemo;

 1. Kuhakikisha Mbadawati ya Jinsia katika Vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu yanazinduliwa kama ilivyobainishwa na muongozo aliouzindua siku hiyo.
 2. Kuanzisha madawati ya jinsia hadi kwenye shule za msingi na sekondari,
 3. Wizara kushirikiana na wadau kufanya mapitio ya Sheria na Sera ili kuleta usawa wa kijinsia.

Ndugu Wananchi, Serikali katika kutekeleza maagizo hayo kwa upande wa Shule za Msingi na Sekondari imeandaa na kusambaza Mwongozo wa Uanzishwaji wa Madawati kwenye ngazi hizo. Kwa Vyuo vya Elimu ya Juu jumla ya Madawati 22 ya jinsia yameanzishwa. Vilevile nimejulishwa kuwa katika Kampeni hii ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia nchini, vyuo vitatu (3) vitazindua madawati ambavyo ni Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya, Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mbeya (MCHAS) na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Chuo Kikuu Dar es Salaam, Kampasi ya Mbeya (UDSM-MCHAS).

Nawapongeza Wakuu wa Vyuo vilivyokwisha zindua madawati na tumeanza kuona manufaa ya madawati haya kwenye vyuo. Wito wangu kwa vyuo vilivyobaki tuharakishe uanzishwaji wa madawati haya na tusijiwekee mazingira magumu ya kuanzishwa kwake, turahisishe mazingira tutaendelea kuboresha, suala la kulinda wanafunzi dhidi ya huu ukatili wa kijinsia lichukuliwe ni DHARURA kwani akikatiliwa leo anaathirika moja kwa moja.

Ndugu Wananchi, Kama nilivyosema awali kuwa, kwenye kupambana na Ukatili wa Kijinsia, pamoja na kuungana, ubunifu haukwepeki na uhusika wa jamii yenyewe nao haukwepeki na ni muhimu kwenye kufikia suluhisho la kudumu.  Ninafahamu katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu pale jamii iliposhirikishwa na pale ubunifu wa jamii ulipopewa nafasi matunda mazuri yameanza kupatikana.

Matunda haya pia ni matokeo ya kuwashirikisha na kuwahusisha siyo wananchi tu bali na viongozi wa kijamii kama vile viongozi wa dini, viongozi wa kimila, wazee maarufu na watu wengi ambao wana sauti katika jamii husika.

Ni katika kutambua umuhimu wa jamii na kila mtu mmoja mmoja Serikali kupitia Wizara ninayoiongoza iliamua kuboresha mwelekeo wa Kampeni ya Msingi ya kutokomeza Ukatili huu ijulikanayo kama Twende Pamoja Ukatili Tanzania sasa basi ambapo, maboresho haya yalitupeleka kwenye kuitisha jamii itekeleza Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) iliyozinduliwa rasmi tarehe 16 Juni, 2022. Mashujaa hawa wanakwenda kwa kaulimbiu ya Kataa Ukatili wewe ni Shujaa ambapo, hadi Oktoba 2022, jumla ya watu 9,245 (9,065 Tanzania Bara na 180 Zanzibar) wamejiunga na Kampeni hiyo.

Ndugu Wananchi, Kampeni hii ni Huru, ya kizalendo na kila mmoja anakaribishwa kujiunga na asili yake ni moyo wa kujitolea kuelimisha na kuhamasisha jamii kupiga vita Ukatili wa Kijinsia. Aidha, Kampeni ya SMAUJATA inalengo la kuongeza nguvu na kasi ya Kupambana kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto na jamii ili kufikia malengo ya Kitaifa. Nichukue fursa hii kumpongeza sana Ndg Sospeter Mosewe Bulughu, kijana mzalendo mwenye moyo wa kujitoa ambaye tulimteua aratibu jamii ihamasike na ijitokeze kujiunga na Kampeni hii, Hakika, yeyé na wasaidizi wake wamefanya kazi nzuri na wanastahili kutambuliwa sambamba na kila aliyeshiriki na zoezi la kuwatambua tutalifanya kwenye usiku wa SMAUJATA ambao tutaandaa kipekee hivyo, kila shujaa atatambuliwa kwa ushujaa wake, mwongozo utatolewa.

Ndugu Wananchi, Nimefahamishwa kwamba kwa uzito wa Kampeni za mwaka huu, mmeandaa programu mbalimbali zikiwemo Msafara wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia ambapo mimi mwenyewe nitauzindua leo hapa uwanjani. Lengo la msafara huu ni kufikia jamii, mtu binafsi, wanafunzi na kuhamasisha mbinu mbalimbali za kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia. Niwaahidi kuwa mimi nitashiriki kwenye baadhi ya mikoa ambayo msafara utapita. Aidha, nawapongeza kwa kuona umuhimu wa kuongeza hamasa ya kuchochea mabadiliko katika jamii zetu ambapo mmeandaa siku maalum ya kutoa tuzo kwa vinara wa kuzuia vitendo vya ukatili. Nawapongeza kwa dhati kwa hatua hiyo kubwa ya kuendeleza juhudi za Serikali katika kupinga ukatili wa kijinsia nchini. Natoa wito kwa mamlaka za mikoa, kuupokea msafara huu na kuendeleza yale mazuri yatakayoonekana kwenye msafara huu yashuke hadi ngazi ya jamii kila mtaa, kila kijiji kwani bila kufanya hivyo, hatutagusa wananchi.

Ndugu Wananchi, Nawahakikishia kuwa, mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto ni vita endelevu hivyo, Siku hizi 16 zitatumika pia kufanyia tathmini maeneo yote yanayohusiana na ukatili wa kijinsia ili kubaininsha kiwango cha tatizo tulilo nalo na kupendekeza mikakati ambayo wadau wote wanaweza kuitumia katika kushughulikia tatizo hili katika mazingira ya eneo husika. Serikali iko tayari kupokea mrejesho wa maazimio mtakayoyafikia baada ya Kampeni hii ya Siku 16 na kwa pamoja, tutafanya mpangokazi shirikirishi ili kujibu utekelezaji wa mapendekezo hayo.

Aidha, tutafanya na tathmini ya jinsi gani kila mkoa, wilaya, halmashauri, tarafa, kata, mtaa na kijiji ulishiriki kutekeleza Kampeni hii kama ilivyoelekezwa na matokeo tutayachapisha na kuyatangaza ili kila mfumo uone hali ya uhai wake kwenye vita hii inayomhusu kila mmoja kwa nafasi yake. Vilevile, tutafanya tathmini ya kuona jinsi gani mitandao yote ya kijamii mathalani ; SKAUTI, SMAUJATA, Vijana, Wazee, Wazazi, Wanawake, Watoto, Mitandao ya Wanaume na mingine inapigana kwa ushirikiano na Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto.  Lengo ni kujengeana uwezo ili sambamba na jukumu la msingi la mtandao husika pia waitendee haki ajenda ya kutokomeza ukatili huu wa kijinsia na kwa watoto kwani ; hatuwezi kushinda bila umoja na uratibu makini wa nguvu ya jamii.

Ndugu Wananchi, Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kwa mara nyingine kushukuru WiLDAF na Wadau wote walioshiriki kufanikisha uzinduzi huu. Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kwamba Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati Dhidi Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka 2022 imezinduliwa rasmi leo tarehe 25 Novemba, 2022 kwenye viwanja vya Leaders Klabu, Jijini Dar es salaam.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Back To Top