skip to Main Content

Miaka 25 ya Kutumia Sheria Kuboresha Maisha ya Wanawake

HOTUBA YA MWENYEKITI WA WiLDAF KWENYE KUMBUKIZI YA MIAKA 25 YA KUANZISHWA KWA WILDAF TANZANIA

Tarehe: 20, Oktoba 2022

Eneo: Hoteli ya Serena- Dar es Salaam

  1. Salaam

Ndugu Mgeni Rasmi,

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan;

Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Wakili. Damas Ndumbaro, (MB);

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima, (MB);

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Amos Makalla;

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary G. Makondo;

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula;

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

Balozi wa Ireland, Mheshimiwa Mary O’Neill;

Balozi wa Norway, Mheshimiwa Elisabeth Jacobsen;

Mratibu Mkazi kutoka Umoja wa Mataifa, Kitengo cha Wanawake, ndugu Hodan Addou;

Mkurugenzi wa Misheni ya Shirika la Msaada la Watu wa Marekani, Bi. Kate Somvongsiri;

Mkurugenzi wa Shirika la Huduma za Msaada wa Kisheria (LSF), Bi. Lulu Ng’wanakilala;

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya mliopo;

Viongozi Waandamizi kutoka Mahakamani;

Viongozi Waandamizi kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali;

Wawakilishi kutoka Balozi na Mashirika ya Kimataifa nchini;

Viongozi wa Madhehebu ya Dini,

Wawakilishi kutoka Taasisi na Asasi mbalimbali hapa Nchini;

Waandishi wa Habari;

Wageni waalikwa;

Mabibi na Mabwana,

  1. Utangulizi

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kuiona siku hii ya leo. Kwa niaba ya Wanachama, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa WiLDAF, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kukubali mwaliko wetu wa kuungana nasi katika kusherehekea miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) hapa nchini. Hakika, hii inadhihirisha  dhamira yako ya dhati ya kutetea haki za wanawake ili kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Kauli mbiu  ya maadhimisho yetu ni;

“Miaka 25 ya Kutumia Sheria Kuboresha Maisha ya Wanawake”.

Sote tunafahamu kuwa Sheria ni nyenzo muhimu katika kuleta Mabadiliko. Ikitumika vizuri, Sheria inabadilisha Maisha ya watu, inalinda haki za watu na inawawajibisha wale wanaovunja. Ni kutokana na msingi huo mkubwa, Shirika la WiLDAF liliamua kutumia Sheria kama nyenzo ya kuwainua Wanawake katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii. 

  1. Chimbuko la WiLDAF

Ndugu Mgeni Rasmi,

Ninaomba uniruhusu  nikufahamishe kidogo kuhusu historia ya WiLDAF. Mtandao wa WiLDAF ulianzishwa nchini Zimbabwe wakati wanawake wengi wao wakiwa wanasheria wakijiandaa kuhudhuria mkutano wa Beijing wa Mwaka 1995. Wanawake hao waliona ipo haja ya kuwa na mkutano wa pamoja ili kujadili changamoto za kisheria ambazo wanawake wa Afrika wamekuwa wakikumbana nazo. Ni kutokana na Mkutano huu wa Harare, Zimbabwe wa mwaka 1994, WiLDAF ilizaliwa katika nchi kumi na tano barani Afrika na baadae kusambaa katika nchi 26 barani Afrika. Wanawake hawa waliona tatizo kubwa linalowakabili wanawake barani Afrika ni sharia za kimila kitaifa na hata kimataifa ambazo zimekuwa zikitumika kuwakandamiza wanawake. Hata hivyo, waliona ipo haja  kupitia mkutano wa Beijing uliokuwa unaandaliwa kutumia fursa ya kupiginia haki za wanawake kwa kuhamasisha maboresho ya sheria ili wanawake waweze kupata fursa na kufaidi rasilimali zilizopo.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Kwa hapa Tanzania, WiLDAF ilisajiliwa rasmi mwaka 1997. Mara tu baada ya kusajiliwa WiLDAF ilianza safari ya kuchochea Mabadiliko ya Sheria ya Kimila ya Mirathi,Tangazo la Serikali Namba 358 la Mwaka 1963 ambazo ni kandamizi kwa wanawake na wasichana. Hii ilikuwa ni ajenda ya kwanza ya WiLDAF. Baadae WiLDAF iliendelea kuchochea mabadiliko ya sheria na mifumo ambayo inakandamiza wanawake.

  1. Mafanikio

Ndugu Mgeni Rasmi,

Katika kumbukizi ya miaka 25, WiLDAF tunajivunia kuwa sehemu ya kuchangia mabadiliko makubwa ya sheria na sera zinazolenga kuleta usawa wa kijinsia na kuwatetea wanawake na watoto kutoka katika mila, desturi na tamaduni kandamizi. Baadhi ya Sheria hizo ambazo tumeshiriki moja kwa moja au kupitia wanachama kutoka mitandao yetu ni pamoja na; Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998 ambayo imeingizwa katika Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sheria ya Ardhi ya mwaka na Sheria ya Ardhi ya Vijiji za mwaka 1999, ambazo WiLDAF tulishiriki tukiwa bado wachanga kabisa. Vilevile Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, Sheria Dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu ya mwaka 2008, Sheria ya UKIMWI ya mwaka 2008, na Sheria ya Haki za Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010.

Kipekee kabisa, WiLDAF tumeshiriki kwa karibu sana katika michakato yote ya utungwaji wa Sheria ya Huduma za Msaada wa Sheria ya mwaka 2017, ambayo imeleta mapinduzi makubwa katika kutambua wasaidizi wa kisheria ambao WiLDAF imekuwa sehemu ya uanzishwaji wao. Pia Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 ambayo imeongeza masuala ya Jinsia na ujumuishwaji wa makundi maalum.

WiLDAF pia tumeshiriki katika utungwaji wa Sera na Mipango ya Serikali, mathalani, mabadiliko ya Fomu namba 3 ya Polisi maarufu kama “PF3, Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Vitendo vya Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) 2017-2022, Mwongozo wa Uanzishwaji, Uendeshwaji na Ufuatiliaji wa Madawati ya Jinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu na Kati Nchini na mchakato wa utungwa wa Sera ya Jinsia.

Sambamba na hayo, WiLDAF tunajivunia kufanya kazi na jeshi la polisi na kuwa kinara wa uanzishwaji wa Madawati ya Polisi ya Jinsia na Watoto pamoja na Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Mafanikio haya ambayo WiLDAF leo tunajivunia hayangekuwa rahisi isipokuwa kwa ushirikiano wa wadau  wa Maendeleo ambao wametushika mkono katika safari yetu ya kutetea haki za Wanawake. Ingawa si rahisi kuwataja kila mmoja, ninaomba uniruhusu niwataje wafuatao;

Shirika la Msaada la Watu wa Marekani kupitia Freedom House/Pact pamoja na Shirika la Huduma za Msaada wa Sheria (LSF), ambao wamekuwa nasi kwa muda mrefu na pia kusaidia kufanikisha kumbukizi hii. Aidha, ninaomba niwashukuru wadau wa maendeleo, ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia WiLDAF na kazi zake za kuhudumia jamii. Hawa ni pamoja na; Balozi za nchi za Finland, Denmark, Ireland, Sweden, Marekani, na Switzerland; Umoja wa nchi za Ulaya (EU); UN Women, UNFPA na ILO; Pia ninayashukuru mashirika ya ndani na nje kama; FCS, Save the Children, Voice Global, AWDF, Raising Voices, Women Fund Trust, MEDA, na Action Aid.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Kipekee naomba niwashukuru Shirika la Msaada la Watu wa Marekani (USAID) na Shirika la Msaada la Watu wa Ireland (Irish Aid) ambao wametembea nasi zaidi ya miaka 10 kutetea haki za wanawake na usawa wa kijinsia.

  1. Maombi yetu

Ndugu Mgeni Rasmi,

Pamoja na mafanikio makubwa ambayo tunajivunia, bado kuna changamoto nyingi katika Sheria ambazo zimekuwa ni kikwazo kwa Wanawake kupata haki zao, kumiliki mali na kushiriki shughuli za kiuchumi na kuinua pato la taifa. Hivyo basi,

sisi Wanachama, Bodi ya Wakurugenzi,Menejimenti na Wafanyakazi wa WiLDAF, kwa heshima na taadhima, tunakuomba utusaidie kufanyia kazi masuala yafuatayo:

  • Kuharakisha wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971

Sheria hii imedogosha sheria zingine kama vile Sheria ya Elimu na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009. Wakati Sheria ya Elimu pamoja na kanuni za adhabu sura ya 16 zinakataza mtoto wa chini ya miaka 18 kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na imetoa adhabu kali kwa wote watakao jihusisha na mahusiano ya kimapenzi, sheria ya ndoa imehalalisha watoto wa umri huu kuolewa na hivyo kusababisha kuwa inatumika kama kichaka pale mtu anapokutwa na hatia ya kosa hilo.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Ucheleweshaji wa mabadiliko ya sheria hii, umeendelea kusababisha watoto wakike kuolewa katika umri mdogo na kukumbana na ukatili wa kijinsia kwa sababu ya kushindwa kuhimili mikiki ya ndoa.

Tunatambua kwamba Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ipo kwenye mchakato wa kukusanya maoni ya wadau juu ya umri wa mtoto wa kike kuolewa. Hata hivyo, tunaona kuwa mchakato huu unachukua muda mrefu.

  • Kufutwa kwa Sheria za Kimila za Mirathi

Sheria za kimila za mirathi zimekuwa mwiba kwa wanawake na watoto wa kike hapa nchini kufurahia haki yao ya umiliki wa mali na ardhi ya ukoo. Sheria hii inasababisha wanawake kuwa maskini na tegemezi kwa mali waliyoitolea jasho na wenzi wao maisha yao yote, hivyo kushindwa kujiwekeza na kujitegemeza kiuchumi.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Itakumbukwa kwamba Sheria hizi za kimila zilitamkwa kuwa zinakiuka haki za wanawake na watoto wa kike kuhusiana na kurithi kama zinavyolindwa na Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) katika shauri la E.S. & S.C. dhidi ya Tanzania, CEDAW/C/60/D/48/2013, katika uamzi wa kamati ya kusimamia mkataba huu uliotolewa mnamo tarehe 2 Machi 2015. Hata hivyo, pamoja na kupewa miezi 12 kuanzia siku ya uamuzi huu kuzirekebisha, Sheria hizi za kimila, bado zinaendelea kufanya kazi. Ni dhahiri kwamba Sheria hii kandamizi ya Mirathi, inahujumu jitihada zako za dhati za kuimarisha haki za kiuchumi kwa wanawake kupitia jukwaa la kizazi chenye usawa, ambapo mimi ni mmoja wa wajumbe wa kamati yako uliyoiteua ili kuhakikisha nchi inafikia malengo iliyojiwekea ya ushiriki wa wanawake kiuchumi.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Itakumbukwa pia kwamba mabadiliko ya Sheria hizi zilizopitwa na wakati  za Mirathi za Kimila, imekua ni ombi la muda mrefu la WiLDAF kupitia Kikosi cha Kutetea Haki za Mirathi (KIKUHAMI). Toka mwaka 2000, WiLDAF, kama mratibu wa KIKUHAMI, tumekutana na viongozi mbalimbali na kuwasilisha rasimu ya Sheria Mbadala (Alternative Bill) yenye mrengo wa jinsia pasipo mafanikio. 

Ndugu Mgeni Rasmi,

WiLDAF, kama mdau wa haki za wanawake na watoto, hatuoni sababu ya kumnyima mwanamke na mtoto wa kike kurithi mali hususani ardhi ambayo ni rasilimali muhimu katika kujiimarisha kiuchumi.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Sheria hii haiathiri wanawake na mabinti tu kama wengi wanavyodhani, bali pia watoto wa kiume ni wa hanga pale mama zao wanaponyang’anywa mali na kutelekezwa. Hivyo, ni wazi kwamba mabadiliko ya Sheria ya Mirathi siyo ajenda ya wanawake tu bali ya watu wote. Hivyo, ni rai yetu, Mhe. Mgeni Rasmi, kuwa wakati sasa umefika kufanya mabadiliko ya sheria hizi za kimila ili ziruhusu haki sawa ya kurithi kwa wanawake na watoto wa kike.  Kama mshiriki wa harakati hizi kwa miaka mingi, tangu Beijing, uwingi wa wanawake wa vizazi vyote uliowakilishwa hapa, ni nguvu ya kukutia moyo kwani wakati wa mabadiliko ni sasa na kwamba unalo jeshi kubwa nyuma yako katika harakati hizi. Tuna imani nawe kuwa mabadiliko yanawezekana.

  • Mapitio na Maboresho ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi ya Taifa

Ndugu Mgeni Rasmi,

Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 yaliweka masuala ya jinsia na ujumuishwaji.

Hata hivyo, Sheria ya Vyama vya Siasa haijaweka takwa la kisheria kuvitaka vyama vya siasa kuzingatia usawa wa kijisia. Pia,  Sheria ya Uchaguzi ya Taifa haijaweka utaratibu fanani wa kuwapata wanawake wabunge na madiwani kwa nafasi za viti maalumu. Hii inapelekea vyama vya siasa kutokuzingatia usawa wa kijinsia wakati wa uchanguzi ndani ya vyama pia uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi. Sambamba ya hayo, bado Sheria ya Uchaguzi ya Taifa haitambui vitendo vya ukatili wa kijinsia kama moja ya kosa la uchaguzi. Hali hii inadhoofisha ushiriki wa wanawake katika siasa kwa hofu ya kunyanyaswa kijinsia.  Shuhuda za wanawake waliopata madhira mbali mbali wakijaribu kuwania nafasi za uongozi zinatukumbusha wajibu wetu kama watetezi wa haki za wanawake katika uongozi na siasa.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Tunatambua na kuthamini namna ambavyo umekuwa kinara wa usawa wa kijinsia katika nyanja zote ikiwemo siasa. Kwa unyenyekevu mkubwa uniruhusu kutumia fursa hii kukuomba uache legacy katika eneo hili la usawa wa kijinsia katika siasa kwa Serikali kuboresha Sheria ya Vyama Vya Siasa ya mwaka 2019 na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010, ili Sheria hizi mbili zitoe maelekezo kwa Vyama Vya Siasa kuwa katika kila Chaguzi za ndani na nje ya Vyama angalau asilimia 50 ya wagombea wawe wanawake na pia Sheria hizi mbili zitambue ukatili wa kijinsia mtandaoni kwa wanawake wanasiasa kama makosa yasiyokubalika na adhabu kali iwekwe. Mhe Rais, habari njema ni kwamba kazi hii imeshaanza kwa maana ya Wizara ya Katiba na Sheria imeanza kufanyia kazi eneo hili kufuatia kuwasilishwa Bungeni na Mhe Neema Lugangira katika Bunge la Bajeti mwaka huu 2022. Pia tumeona utayari mkubwa kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo tumekuwa tukishiriana nayo katika mazingira bora ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa. Tukufahamishe tu kwamba, hivi sasa kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili pamoja na Baraza la Vyama vya Siasa tumeweza kushirikiana kutengeneza Sera za Jinsia kwa vyama nane, ikiwemo chama chako cha CCM.

  • Haja ya Kutungwa kwa Sheria inayoshughulikia masuala ya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto

Ndugu Mgeni Rasmi,

Tatizo la ukatili wa kijinsia bado ni kubwa nchini. Tunatambua jitihada za dhati za Serikali katika kuimarisha Sheria, Sera na Mifumo ya kukabiliana na janga hili, ikiwa ni pamoja na uanzishwaji na uimarishwaji wa madawati ya polisi ya jinsia na watoto, Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), Uanzishwaji na uimarishwaji wa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika ngazi ya kata, wilaya na mkoa, uanzishwaji wa vituo vya mkono kwa mkono, uanzishaji wa kitengo cha mahakama jumuishi na utekelezaji wa afua mbalimbali zinazolenga kuzuia na kusaidia wahanga wa ukatili wa kijinsia.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Hata hivyo, kutokana na kukosekana kwa sheria mahususi ya kushughulikia ukatili wa kijinsia, uendeshaji wa mashitaka  yanayohusiana na ukatili wa kijinsia umekuwa ukigubikwa na mapungufu kadhaa ikiwemo kesi kuchukua muda mrefu sana. Hivyo, ni rai yetu kwamba wakati sasa umefika kuwepo na sheria mahususi itakayoshughulikia masuala ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto (comprehensive GBV law) kwa muktadha huu.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Wakati tukiadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa WiLDAF, ninapenda kuwashukuru na kuwapongeza kina mama hodari na waanzilishi wenzangu wa WiLDAF ambao ni Balozi, Dr. Asha Rose Migiro, Dr. Judith Odunga, Dr. Hellen Kijo Bisimba na Wakili Nakazael Tenga. Katika vuguvugu la kutetea haki za wanawake na kuhakikisha wanapata msaada wa kisheria, viongozi hawa walitumia fursa vizuri ikiwa ni pamoja na kushiriki katika mikutano ya kimataifa na kikanda inayohusu haki za wanawake. Ni kutokana na ushiriki wao waliweza kuja na wazo la kuanzisha shirika la WiLDAF kama sehemu ya mtandao kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Pia ninapenda kuwashukuru na kutambua mchango mkubwa ya Bodi ya Wakurugenzi (iliyopo na zilizopita), Menejimenti na Wafanyakazi  ambao kwa asilimia 70 ni vijana wanaochipukia. Nikiwa mmoja wa waanzilishi wa WiLDAF na harakati za haki za wanawake nchini ninajivunia kuona kizazi kipya chenye ari na kasi katika kuhakikisha wanaendeleza yale tuliyoyaanza na hatimaye kuwa na jamii ambayo wanawake na wanaume wanawaweza kufikia na kutumia fursa mbalimbali zilizopo ili kujikwamua kiuchumi kwa mustakabali wa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Naomba nitambue mchango wa wanachama wote wa WiLDAF na mitandao ambayo WiLDAF imekuwa ikiiratibu kama vile Mtandao wa Kupinga Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia (MKUKI), Kikosi cha Kutetea Haki za Mirathi (KIKUHAMI), Mtandao wa Wakurugenzi Wanawake wa Asasi za Kiraia, ambao kwa kiasi kikubwa wamewezesha ufikiwaji wa watu wengi hasa wanawake na matokeo zaidi kwenye shughuli ambazo WiLDAF imekuwa ikiratibu.

Ndugu Mgeni Rasmi,

Kwa umuhimu mkubwa, ninapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali yetu kwa ushirikiano ambao tunaendelea kuupata katika kukuza usawa wa kijinsia na kuimarisha haki za wanawake. Ni wazi kwamba, mafanikio tunayojivunia leo yasingewezekana ikiwa Serikali haingeweka mazingira wezeshi ya kufanya kazi na asasi za kiraia ili kuwaletea wananchi maendeleo. Aidha, tunatambua mchango mkubwa wa Wizara ya Sheria na Katiba, chini ya Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, kwa kuwa tayari kushirikiana nasi na kujadiliana namna ya kuboresha sheria mbalimbali kwa lengo la kuwainua wanawake kwenye nyanja zote za maisha hapa nchini.

Tunaishukuru pia Wizara ya Kisekta, ambayo ni wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, chini ya Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, kwa kazi zao nzuri na ushirikiano mkubwa wanaoendelea kutupatia kwetu sisi na asasi nyingine za kiraia.

Kwa kipekee kabisa, Mhesimiwa Rais, hapa tunakupongeza sana wewe binafsi kwa kuirejesha wizara hii maalum inayohusika na masuala ya jamii, wanawake na jinsia. Sote tunashuhudia namna hatua hii imesaidia kuleta msukumo wa utekelezwaji wa ajenda za wanawake na jamii kwa ujumla ndani ya Serikali. Tunamwona Waziri wetu akitoka ofisini na kushiriki shughuli za kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu masuala ya maendeleo. Sisi WiLDAF ni miongoni mwa mashirika ya kwanza aliyopata kutembelea mara tu alipokabidhiwa wizara hii. Na hivi jana tu, ameshiriki uzinduzi wa ofisi za ‘Shirika la Sauti ya Jamii Kipunguni’ ambalo WiLDAF ilichangia uanzishwaji wake na linafanya kazi nzuri ya uhamasishaji jamii kuhusiana masuala ya usawa wa kijinsia.

 

Ndugu Mgeni Rasmi,

Tunaendelea kutoa shukrani zetu za dhati kwako kwa uhodari na uongozi mahiri katika kutuletea maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla, kwa hakika umekuwa kielelezo tosha na mfano kwa wanawake na mabinti wote. Tunatoa shukrani na pongezi kwa kuridhia kuwa championi wa haki za kiuchumi za wanawake kupitia jukwaa la kizazi chenye usawa. Sote tunatambua, utegemezi wa kiuchumi ni moja wa vyanzo vikuu vya ukatili na ukandamizwaji dhidi ya wanawake. Na sisi kama WiLDAF tumelizingatia hili na kujumuisha haki za kiuchumi katika mpango mkakati wetu wa miaka mitano ambao tunakaribia kuanza kuutekeleza. Wakati tunaahidi kuendelea kushirikiana nawe bega kwa bega kuhakikisha tunatokomeza umasikini nchini, kama ulivyojionea hapa kazi uliyoianza na wanawake wenzako miaka mingi iliyopita, vugu vugu lake halitapoa kwani tunao wanawake rika lote walio tayari kushirikiana nawe katika kuleta ukombozi wa wanawake kisiasa, kiuchumi na kijamii kupitia sheria.

WiLDAF tuko pamoja nawe, tunakutakia hekima na busara na kila la kheri katika uongozi wako.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki Raisi wetu Samia Suluhu Hassan.

Ahsanteni kwa kunisikiliza

 

Imetolewa na:

Dr. Monica Mhoja

(Mwenyekiti)

Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF)

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Back To Top