skip to Main Content

Press Release

UZINDUZI WA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA, 2020

Ndugu Wanahabari;

Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) ambao unaratibiwa na WiLDAF kwa kushirikiana na, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia wazee Wazee na Watoto na wadau wa maendeleo, wakiwemo UN Women, UNFPA, LSF, Save the Children na Balozi mbalimbali tunaungana na wanaharakati wote duniani kuadhimisha kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia. Kampeni hii inatarajiwa kuanza rasmi tarehe 25 Novemba mpaka tarehe 10 Desemba.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni;

Tupinge Ukatili wa Kijinsia:

Mabadiliko Yanaanza na Mimi’.

Ndugu Wanahabari,

Kauli mbiu hii inatoa wito kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia ambalo ni tatizo kubwa nchini Tanzania na duniani kwa ujumla.

Tafiti mbalimbali zinaonesha ukubwa wa tatizo mathalani ripoti ya utafiti wa Afya na Hali ya Watu Tanzania ya mwaka 2015-2016, inaonesha kuwa asilimia 40 (40%) ya wanawake na wasichana wenye umri kati ya miaka 15-49 wamepitia ukatili wa kimwili katika Maisha yao.

Kwa upande wa ukatili wa kingono, Ripoti ya Polisi juu ya makossa dhidi ya utu iliyotolewa mwaka 2019, imeonesha kuwa kati ya matukio 11,759 yaliyoripotiwa, mwaka 2018 matukio 7,617 yalikuwa ni makosa ya ubakaji ambayo ni sawa na asilimia 64.7.

Rushwa ya ngono, hususan katika vyuo vikuu imekuwa ni tatizo kubwa. Ripoti ya utafiti uliofanywa na Takukuru katika chou kikuu cha Dar es salaam na chuo kikuu cha Dodoma inaonesha zaidi ya asilimia 50 ya wahojiwa walieleza uwepo wa ngono katika vyuo vikuu.

Ndugu wanahabari

Tafiti zinaoonesha kuwa vitendo hivyo vinafanywa na watu wanaofahamika na wahanga wakiwemo wapenzi, watu wa karibu, marafiki na watu wenye mamlaka.

Hivyo basi, kauli mbiu ya mwaka huu inamtaka kila mtu kuchukua hatua za kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia, kuhakikisha kuwa sauti za wahanga na wanaharakati zinasikika ili kukomesha vitendo vyote vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto.

Pamoja na mambo mengine, kampeni ya mwaka huu imeangazia katika maeneo matano ambayo ni ukatili majumbani, ubakaji, ndoa za utotoni, ukatili dhidi ya wenza (intimate partners violence) na rushwa ya ngono.

Ndugu wanahabari

Katika kipindi hiki cha kampeni ya siku 16, za kupinga ukatili wa kijinsia kutakuwa na shughuli mbalimbali. Shughuli hizi ni pamoja na siku ya wahariri ambayo imeandaliwa leo hii ili kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari katika kuongeza uelewa wa maswala ya ukatili wa kijinsia, takwimu za ukatili na jinsi ya kuandaa ripoti za kesi za Ukatili wa Kijinsia.

Vile vile kutakua na msafara wa kupinga ukatili wa kijinsia (Caravan Route) utakaopita mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe na Mbeya, walengwa wakuu katika msafara huu ni wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu katika mikoa husika pamoja na wananchi wa maeneo hayo.

Kutakuwa na siku ya kutoa Tuzo kwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia, pia kutakua na midahalo mbali mbali juu ya maswala mtambuka yanayohusu ukatili wa kijinsia pamoja na shughuli nyingine zitakazoendelea kufanyika katika kipindi chote cha kampeni ndani ya siku zote kumi na sita 16 za kampeni.

Hali kadhalika, wanachama wa MKUKI watakuwa na shughuli mbalimbali kipindi chote cha kampeni.

Ndugu wanahabari;

Mwisho kabisa tunatoa wito kwa jamii, viongozi wa dini, taasisi na idara za serikali, asasi za kiraia, taasisi binafsi pamoja na wanahabari kupaza sauti, kuchukua nafasi katika kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia. Kila mtu awe sehemu ya mabadiliko, kwa pamoja kupitia kauli mbiu ya mwaka huu tunasisitiza;

‘Tupinge Ukatili wa Kijinsia:

Mabadiliko Yanaanza na Mimi’

Tufatilie kupitia mitandao yote ya kijamii (Facebook, Twitter, Instagram) @16DaysTanzania, @wildaftz

Asanteni kwa kunisikiliza!!!!

Imetolewa na;

Anna M. Kulaya (Mratibu wanchi (WiLDAF)

Kwa niaba ya: Mtandao wa kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) unaojumuisha asasi zaidi ya 100 zinazotetea haki za Wanawake na usawa wa kijinsia nchini,

S.L.P 76215, Dar es Salaam.

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Back To Top