WiLDAF pamoja na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) wanaandaa Tuzo za Vinara…

Uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia
HOTUBA YA MKURUGENZI WA WiLDAF KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU 16 ZA UANAHARAKATI DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA TAREHE 25/11/2022
VIWANJA VYA LEARDERS CLUB KINONDONI, DAR ES SALAAM.
- Mheshimiwa Dkt Doroth Gwajima Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (Mbunge).
- Naibu Katibu Mkuu Dkt. Amon Mpanju – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum.
- Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe.
- Mwenyekiti wa Bodi ya WiLDAF Dkt. Monika Magoke Mhoja.
- Balozi wa Denmark Mette Spandent
- Balozi wa Finland, Thereza Zitting .
- Balozi wa Ireland Mary O’Neill
- Balozi wa Canada Kyle Nunas
- Balozi wa Belgium Peter Huyghebaert
- Balozi wa Uholanzi Wiebe de Boer
- Zlatan Millisic Muwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Tumekusanyika hapa leo tukiungana na mataifa mengine kote duniani kuadhimisha Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia ambapo kitaifa unaizindua wewe mwenyewe leo hapa katika viwanja vya Klabu ya Viongozi (Leaders Club) . Leo ni siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake ambayo ndio siku ya kwanza katika kuadhimisha kampeni ya siku 16 za Uanaharakati.
Ingawa tunafuraha kuona umati mkubwa huu na wewe mwenyewe mgeni rasmi ukijumuika nasi kwenye uzinduzi huu, mioyoni tumejaa machungu tele. Ni hali ya kusikitisha kuwa karne hii ya 21 ya ulimwengu uliostaarabika, bado kuna matukio ya ukatili wa kijinsia kwani tunaamini yanazuilika.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kauli mbiu ya kampeni ya mwaka huu ni
“Kila Uhai Una Thamani! Tokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.”
Kauli mbiu hii imelenga kuhamasisha kila mtu, jamii, taasisi na serikali kuwa sehemu ya kuwajibika kutokomeza vitendo vyote vya ukatili kwani madhara yake ni makubwa na mwisho hupelekea vifo hasa kwa wanawake na wasichana.
Sisi Wana Mtandao wa MKUKI unaoratibiwa na WiLDAF tumeamua kuangazia ukatili unaofanyika nchini ambao mwisho wa siku unapelekea madhara makubwa ya kiuchumi, kisaikolojia, kiafya na hata vifo.
Kwa miaka ya hivi karibuni sisi wana MKUKI tumekuwa tukishuhudia kupitia vyombo vya habari au kupokea kesi katika vituo vyetu na taasisi zetu zinazohusiana ukatili na vifo vya wanawake sababu kubwa ikiwa ni wivu wa mapenzi.
Mathalani Ripoti ya Uhalifu ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2021 inaonesha katika kipindi cha Januari hadi Desemba, jumla ya watu 29,373 walifanyiwa ukatili wa kijinsia. Kati yao wanawake ni 20,897 na wanaume ni 8,476 ambapo kati yao mauaji ya vikongwe ni 118. Asilimia 68.6 ya mauaji yaliyoripotiwa yalikuwa ni dhidi ya wanawake. Mwaka 2020, mauaji yaliyotokana na migogoro ya majumbani na wivu wa mapenzi ni asilimia 26% ya mauaji yote yaliyoripotiwa katika Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi;
Kinachosikitisha zaidi ni kuwa wanaofanya ukatili huu ni watu wa karibu sana na wahanga. Nyumbani ambapo panapaswa kuwa sehemu salama kwa wanawake na watoto, kumekuwa ni shubiri.
Kinachosikitisha zaidi jamii inawafahamu wakosaji na mara nyingine kuwalinda kwa kuamua kumalizia kesi nyumbani au kutotoa taarifa mapema wanapoona vitendo vya ukatili. Hali hii hutoa mwanya kwa watuhumiwa kurudia vitendo hivyo mpaka siku inayopelekea kifo. Hii inaleta madhara makubwa zaidi na hata kifo, pia inarudisha nyuma maendeleo ya nchi na juhudi za serikali katika kuleta maendeleo na kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.
Na ndio sababu sisi wana MKUKI tumedhamiria mwaka huu kwa kushirikiana na Wizara yako kufanya kampeni kubwa itakayoshirikisha kila mtu mmoja mmoja, familia, wazazi na walezi, jamii na taasisi kwa ujumla. Tunatumia kampeni hii kupaza na kukemea vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya wanawake kwani vinazuilika. Jamii bila ukatili na mauaji dhidi ya wanawake inawezekana. Tuvunje ukimya na tuchukue hatua. Kwa pamoja tunaweza kuokoa Maisha ya wanawake na watoto.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
MKUKI na wadau wengine tumejipanga kutumia siku 16 za kampeni kufanya shughuli mbalimbali kuongeza ushiriki wa kila mwanajamii katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Kwa leo utazindua msafara wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia ambao utapita mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyanga, Geita, Mara, na Arusha ukihamasisha jamii kuungana nasi katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Msafara huu utatembelea jamiii, mashuleni, kwenye vituo vya mabasi na maeneo ambayo yanaonesha Kombe la Dunia na kwa kutumia njia hii tutaweza kufikia wanaume wengi zaidi na kuhamasisha mabadiliko ya kifikira, kimtazamo na matumizi mabaya ya mamlaka/power walizonazo katika kulinda wanawake na watoto.
Msafara utatembelea shuleni kujadiliana na watoto, walezi na walimu kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Kwa kutumia bodaboda tutahamasisha wawe mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili, kuokoa wanawake na watoto dhidi ya ukatili.
Mheshimiwa mgeni rasmi, tarehe 8 Desemba tunategemea kuwa na tuzo maalum kwa vinara wanaolinda wanawake, watoto na kuzuia ukatili wa jinsia.
Tuzo hii imeanzishwa na wana MKUKI kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo UNFPA na LSF ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa watu katika jamii zetu wanaofanya kazi kubwa ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mwisho kabisa , msafara utamalizika Arusha siku ya tarehe 10 Desemba ikiwa na siku ya Tamko Rasmi la Haki za Binadamu duniani na hitimisho la kampeni .
Kama tunavyozindua leo, tunaamini kwamba siku ya hitimisho utakuwa nasi kupokea msafara ambao utazindua wewe mwenyewe leo na kupokea maazimio ,visa mkasa, matukio na mikakati ambayo italetwa na msafara wa kupinga ukatili wa kijinsia.
Mheshimiwa mgeni rasmi, wana MKUKI tuna jambo letu na mwenyekiti dada yetu Dkt. Monica Mhoja muda ukifika ataweza kusema nawe, ni nini sisi wanamkuki MKUKI tunategemea kutoka katika wizara yako kama sehemu ya committment ya wizara katika kampeni hii.
Namilizia kwa kusema tena kauli mbiu:
Kila uhai unathamani! Tokomeza mauwaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto!
This Post Has 0 Comments