skip to Main Content

Ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Katika Ofisi za WiLDAF

Mnamo tarehe Februari 28 20222, Mtandao wa Kupinga Ukatili (MKUKI) kwa kushirikiana na WiLDAF tulipata fursa ya kutembelewa na Waziri Wa Maendeleo Ya Jamii, Jinsia,Wanawake Na Makundi Maalum katika ofisi za WiLDAF. Ziara hii ililenga kuangazia fursa na changamoto za utekelezaji wa MTAKUWWA na Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia kutoka kwa wanachama wa MKUKI.

Kupitia ziara hiyo Mhe. Waziri Dorothy Gwajima aliweza kujua kazi mbalimbali ambazo Mtandao wa MKUKI imeweza kuzifanya ikiwa ni pamoja na: Maboresho ya Sheria, Sera na Mikakati ya kutokomeza vitendo vya ukatili ambapo huku WiLDAF ikiwa ni miongoni mwa wadau walioshiriki kikamilifu katika utengenezwaji wa MTAKUWWA; Kuanzishwa kwa madawati ya jinsia ya polisi; Kuongeza upatakanaji wa haki na huduma kwa watendewa wa vitendo vya ukatili.

Pamoja na mafanikio, tuliwasilisha changamoto katika utekelezaji wa kazi ikiwemo; Uwepo wa mila na desturi hasi kwa wanawake; Uwepo wa sheria kandamizi kama vile Sheria ya Ndoa na Sheria za Kimila za Mirathi; Kutokuwepo kwa sheria mahususi ya ukatili wa kijinsia; Kukosekana kwa mifumo ya uratibu na ufuatiliaji baina ya taasisi hasa kwa kuzingatia kwamba ukatili wa kijinsia ni swala mtambuka linalohusisha wadau na sekta mbalimbali.

Tuliweza pia kuwasilisha mapendekezo ya maboresho ikiwemo;

  1. Utungwaji wa Sheria mahususi Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia.
  2. Kwa kushirikiana na Wizara za kisekta kama vile TAMISEMI, kusimamia utekelezwaji wa maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa mara mbili wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati juu ya utengwaji wa fedha za kutosha ili kutekeleza afua za MTAKUWWA kwenye ngazi ya halmashauri. Hii inahusisha pia usimamizi wa mikopo kwa makundi maalum kwa mfumo wa 4:4:2.
  3. Wizara kuona uwezekano wa kuongeza idadi ya maafisa ustawi na kuwajengea uwezo zaidi ili watekeleze kwa ukamilifu afua za MTAKUWWA.
  4. Wizara kukamilisha Mchakato wa Sera ya Jinsia ili iweze kuzinduliwa na kuanza kutumika.

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Back To Top