Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji

Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji

Leo, WiLDAF Tanzania inaungana na dunia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji (FGM), ikiwa ni siku ya kuhamasisha jamii kupinga na kukomesha kabisa vitendo hivi vinavyokiuka haki za wasichana na wanawake. Tunaendelea kuwawezesha wanawake na wasichana, kuwashirikisha wanaume na wavulana kama mabingwa wa mabadiliko, kuimarisha nafasi ya viongozi wa dini na mila katika kupinga ukeketaji, pamoja na kusaidia familia kupata njia mbadala za kiuchumi ili kuachana na mila hii potofu. Je unafahamu chochote kuhusiana na ukeketaji?

Ukeketaji (FGM) ni nini?

Ukeketaji, au Female Genital Mutilation (FGM), ni kitendo cha kukata au kuharibu sehemu za siri za mtoto wa kike au mwanamke kwa sababu zisizo za kitabibu.

Hii ni mila hatarishi inayofanyika katika baadhi ya jamii kwa madai ya utamaduni, lakini kwa kweli ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kwa nini Ukeketaji ni Tatizo Kubwa?

Ukeketaji una madhara makubwa ya muda mfupi na muda mrefu, ikiwa ni pamoja na:

1. Madhara ya Kiafya

  • Kutokwa na damu nyingi
  • Maumivu makali
  • Maambukizi na magonjwa
  • Matatizo wakati wa kujifungua
  • Hatari ya vifo

2. Madhara ya Kisaikolojia

  • Msongo wa mawazo (trauma)
  • Hofu na sonona
  • Kupoteza kujiamini
  • Athari za maisha yote

3. Madhara ya Kijamii

  • Kukatisha masomo kwa wasichana
  • Ndoa za utotoni
  • Kudumisha mfumo dume na ukandamizaji wa wanawake

Ukeketaji ni Ukiukwaji wa Haki za Binadamu

FGM inakiuka haki za msingi za mtoto wa kike, ikiwemo:

  • Haki ya afya
  • Haki ya uhai
  • Haki ya utu na heshima
  • Haki ya kuishi bila ukatili na unyanyasaji

Ndiyo maana Tanzania na dunia nzima zimeweka sheria na mikakati ya kupinga ukeketaji.

Je, Ukeketaji Unaendelea Kwa Nini?

Baadhi ya sababu zinazochangia kuendelea kwa FGM ni:

  • Shinikizo la kijamii na mila
  • Imani potofu kwamba ni sehemu ya utu au ndoa
  • Mfumo dume unaodhibiti miili ya wasichana
  • Umaskini na utegemezi wa kiuchumi kwa wakeketaji

Nini Kifanyike Kutokomeza Ukeketaji?

Ili kufikia jamii salama bila ukeketaji, tunahitaji:

  • Elimu na uhamasishaji kwa jamii
  • Ushiriki wa wanaume na wavulana kama mabingwa wa mabadiliko
  • Ushirikiano na viongozi wa dini na mila
  • Uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake na familia
  • Ulinzi wa watoto wa kike na mifumo ya kuripoti

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *