WiLDAF – Yaendelea Kuongoza Mapambano Dhidi ya Ukeketaji Mara
WiLDAF Tanzania, kupitia mradi wa Achieving Zero FGM in Mara – Jamii Imara, inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ukeketaji (FGM) unatokomezwa kabisa katika Mkoa wa Mara.
Mradi huu wa miezi 18, unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani, unatekelezwa katika wilaya za Tarime, Serengeti na Butiama, ukilenga kubadilisha mitazamo ya jamii, kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto wa kike, na kuwezesha kiuchumi familia zinazokata tamaa kuendelea na ukeketaji.
Mafanikio Makubwa
- Kuimarisha Uelewa Mashuleni kupitia Shule Salama Clubs
WiLDAF imeendelea kuendesha klabu za Shule Salama katika shule mbalimbali, ambapo jumla ya wanafunzi 989 (wasichana 536 na wavulana 453) walishiriki katika mafunzo kuhusu ukeketaji, ukatili wa kijinsia na njia za kuripoti matukio.
Klabu hizi hutumia michezo, sanaa, maigizo na mijadala kama njia bunifu ya kuwafikia vijana.
- Wasichana na Vijana Kupewa Nguvu Kupaza Sauti
Kupitia mafunzo ya maisha (life skills), wasichana na mabinti walio nje ya shule waliweza kuhamasisha jamii kupitia majukwaa ya masoko, kliniki na shule.
Zaidi ya watu 7,092 walifikiwa kupitia mabinti mabalozi wa mabadiliko katika kata sita za mradi.
- Mafunzo ya VCAT Kubadilisha Mitazamo ya Wanawake
WiLDAF iliendesha vikao vya Values Clarification and Attitude Transformation (VCAT) kwa wanawake 124 kutoka vikundi vya kiuchumi, kwa lengo la kuondoa imani potofu zinazochochea ukeketaji.
Matokeo yalionyesha ongezeko kubwa la uelewa kutoka 43.5% hadi 85.2%, na vikundi kuanza kuweka sheria za kupiga marufuku ukeketaji kwenye katiba zao.
- Viongozi wa Dini Kujiunga Rasmi Katika Mapambano
Jumla ya viongozi wa dini 20 (18 wanaume, 2 wanawake) walipatiwa mafunzo maalum na kuandaa mipango kazi ya kutumia majukwaa yao kukemea ukeketaji na kutoa msaada kwa watoto wanaokimbia vitendo hivyo.
- Mabingwa wa Kiume Wafikia Jamii Zaidi ya 4,000
WiLDAF imeendelea kuimarisha ushiriki wa wanaume na wavulana katika mapambano haya. Mabingwa wa jamii walifanikiwa kufikia jumla ya wananchi 4,114 kupitia midahalo ya wazi na kampeni za kuondoa mila kandamizi.
- Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Wasichana (AGYW)
Wasichana 45 walipewa mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha ili kuwawezesha kuwa na mbadala wa kiuchumi na kupunguza utegemezi unaoweza kuchochea mila hatarishi.
Uelewa wao wa masuala ya fedha uliongezeka kutoka 40% hadi 93%.
Changamoto na Mafunzo
Mradi umebaini kuwa ukeketaji bado una mizizi katika mifumo ya kijamii na mfumo dume, ambapo baadhi ya wanawake waliokeketwa huendeleza mila hiyo kama njia ya kupata heshima au nguvu kijamii.
Hivyo, WiLDAF inaendelea kutumia mbinu jumuishi na za kuleta mabadiliko ya kijinsia ili kuvunja mzunguko huu wa kizazi hadi kizazi.