skip to Main Content

HISTORIA YA KAMPENI

Siku 16 za Uanaharakati Dhidi ya Ukatili wa kijinsia ni kampeni kabambe ya kimataifa iliyoanzishwa na Kituo cha Kimataifa cha Wanawake katika Uongozi “Women’s Global Leadership”tokea mwaka 1991.

Chimbuko la Kampeni

Chimbuko la kampeni hii inatokana na vuguvugu la wanaharakati duniani kupaza sauti kukemea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Wanaharakati wengi barani Ulaya, Amerika, Asia na Afrika walijenga nguvu ya pamoja na kuleta msukumo wa kutambulika na kuheshimika haki na ulinzi wa wanawake ili kupunguza vitendo vya ukatili walivyokuwa wakifanyiwa wanawake. Mathalani, mauaji ya kinyama ya wanawake wa Mirabelle yaliyofanyika nchini Dominica mwaka 1960. Kuanzia Novemba 25 mwaka 1991, Umoja wa Mataifa ulitenga siku hii kama siku ya Kimataifa ya kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake. Kampeni ya siku 16 za Uanaharakati Dhidi ya Ukatili wa kijinsia huishia Desemba 10 ambayo
ni Siku ya Kimataifa Kuadhimisha Tamko Rasmi la Haki za Binadamu, ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili dhidi ya wanawake na haki za binadamu na kutia msisitizo kwamba ukatili kama huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Ndani ya siku hizi 16 za kampeni ya uanaharakati zimebeba tarehe za siku zingine za Kimataifa ambazo ni muhimu katika kulinda haki za wanawake. Tarehe hizo ni pamoja na Novemba 29 ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Binadamu Wanawake; Desemba 1 Siku ya UKIMWI Duniani; Desemba 3 Siku ya watu wenye ulemavu; Desemba 6 Siku ya kukumbuka mauaji ya kikatili ya Montreal 1989 ambapo Wanawake 14 waliokuwa wanasomea uhandisi waliuawa na mtu aliyekuwa anawachukia wanawake; Desemba 10 Siku ya Tamko Rasmi la Haki za Binadamu. Hivyo basi siku hizi 16 zinatoa mwanga na msukumo
kwa watu, Serikali, jamii na mtu binafsi kutambua kwamba ukatili dhidi ya wanawake ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Uzoefu wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati Dhidi Ukatili wa Kijinsia Kimataifa

Zifuatazo ni kauli mbiu mbali mbali zilizotumika kwenye maadhimisho ya kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.

 • 1991- 1992 Ukatili Dhidi ya Wanawake huvunja haki za binadamu
 • 1992- 1993 Demokrasia bila haki za Wanawake siyo Demokrasia.
 • 1994 Ufahamu, Uwajibikaji, Vitendo: Ukatili Dhidi ya Wanawake huvunja haki za Binadamu.
 • 1995 Vienna, Cairo, Copenhagen na Beijing: Inaleta Haki za Wanawake Nyumbani.
 • 1997 Dai haki za Wanawake Nyumbani na Ulimwenguni Kote.
 • 1998 Kujenga Utamaduni wa Kuheshimu Haki za Binadamu.
 • 1999 Kutimiza Ahadi ya Uhuru Dhidi ya Ukatili.
 • 2000 Kusherehekea miaka 10 ya Kampeni.
 • 2001 Ubaguzi na Ujinsi: Maliza Ukatili.
 • 2002 Kuunda Utamaduni Unaokataa Ukatili Dhidi ya Wanawake.
 • 2003 Ukatili Dhidi ya Wanawake huvunja Haki za Binadamu. Kuendeleza yatokanayo na Mkutano wa Vienna.
 • 2004 – 2005 Kwa Afya ya Wanawake, Kwa Afya ya Ulimwengu; Acha Ukatili.
 • 2006 Sherehekea Miaka 16 ya Siku 16; Endeleza Haki za Binadamu – Komesha Ukatili Dhidi ya Wanawake.
 • 2007 Madai ya utekelezaji, mapambano na changamoto dhidi ya vikwazo ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.
 • 2008 “Haki za Binadamu za Wanawake ni Haki za Binadamu Wote: Sherehekea Miaka 60 ya Tamko Rasmi la Haki za Binadamu”
 • 2009 “SIKO PEKE YANGU – Mwenye nia Binafsi, Uthubutu na Utayari wa Kuzuia na Kupambana na Ukatili wa Kijinsia
 • 2010 “Pinga Ukatili Kuimarisha Familia”.
 • 2011 “Miaka 50 Ya Uhuru: Pinga Ukatii Wa Kijinsia Kuimarisha Tanzania Huru
 • 2012 “FUNGUKA!Kemea Ukatili Dhidi Ya Wanawake. Sote Tuwajibike”
 • 2013 “FUNGUKA!Tumia Mamlaka Yako, Zuia Ukatili Wa Kijinsia: Boresha Afya Ya Jamii”
 • 2014 FUNGUKA!Pinga Ukatili wa Kijinsia kwa Afya ya Jamii.
 • 2015 FUNGUKA!Pinga Ukatili Wa Kijinsia: Elimu Salama Kwa Wote
 • 2016 FUNGUKA!Pinga Ukatili Wa Kijinsia: Elimu Salama Kwa Wote.
 • 2017 “FUNGUKA!Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto Haumuachi Mtu Salama. Chukua Hatua”
 • 2018 FUNGUKA!Usalama Wake; Wajibu Wangu.
 • 2019 Kizazi Chenye Usawa: Simama Dhidi ya Ubakaji
 • 2020 Mabadiliko Yanaanza na Mimi!

Kwa hapa Tanzania, Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) chini ya uratibu wa Shirika la WiLDAF umekuwa ukiongoza kampeni hii ya uanaharakati wa Siku 16 kwa kushirikiana na Serikali, mashirika mengine yasiyo ya kiserikali, wadau wa maendeleo pamoja na sekta binafsi ili kuleta nguvu ya pamoja kutokomeza vitendo vya Ukatili wa Kijinsia. Aidha viongozi mbalimbali wa kitaifa wameshiriki kama wageni rasmi katika uzinduzi wa Siku 16 za uanaharakati dhidhi ya Ukatili wa Kijinsia. Viongozi hawa ni pamoja na Waziri Mkuu,Mheshimiwa Mizengo Pinda, Mheshimiwa Mary Nagu akiwa Waziri wa Sharia na Katiba, Mheshimiwa Sophia Simba akiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Margreth Sitta akiwa Waziri wa Maendeleo yaJamiiJinsia na Watoto, Dkt. Asha Rose Migiro akiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto na Mheshimiwa Angela Kairuki akiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sharia na
Akiwa Waziri wa Uwekezaji,Mheshimiwa Ummy Mwalimu akiwa Waziri wa Afya, Wazee Jinsia na Watoto na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa.
Ushiriki wa Viongozi hawa pamoja na wengine umeongeza ushirikiano wa serikali na asasi za kiraia katika mapambano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia.

Aidha washiriki wengine katika uzinduzi wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ni kama ifuatavyo: –

 • Idara za serikali
 • Wadau wa maendeleo
 • Tume mbalimbali
 • Vyombo vya habari
 • Mashirika ya dini
 • Asasi mbalimbali
 • Wanafunzi
 • Vijana
 • Vyama vya siasa
 • Jeshi la Polisi
 • Wanawake na wanaume kwa ujumla wao
HISTORIA YA KAMPENI
Back To Top