skip to Main Content

YAH: Maoni ya Wadau Juu ya Adhabu ya Viboko Mashuleni.

YAH: Maoni ya Wadau Kuhusu Tamko la Mheshimiwa William Ole Nasha Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi – Juu ya Adhabu ya Viboko Mashuleni.

Shirika La Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) ni mtandao unaojihusisha na Haki za Wanawake barani Afrika katika kukuza na kueneza mikakati inayounganisha sheria na maendeleo ili kuongeza ushiriki wa ushawishi kwa wanawake katika ngazi za kijamii,kitaifa,kikanda na kimataifa. WiLDAF inaratibu kikundi kazi cha mashirika yanayojihusisha na kutetea haki za wanawake, vijana, watoto na watu wenye ulemavu kupitia mradi wa Ushawishi kwa kutumia takwimu.

Kwa pamoja tunapongeza kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi stadi, Mheshimiwa William Ole Nasha (Mb) akiwa bungeni siku  ya tarehe 13 Novemba 2018 wakati akijibu swali  no 84 toka kwa  Mbunge wa viti maalum Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve. kwamba “hakuna mwalimu yeyote  kutoa adhabu au kutembea na kiboko kinyume na miongozo iliyowekwa na sheria kwa ajili ya kutoa adhabu mashuleni. Pia tunapongeza jitihada za serikali kutambua kwamba vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto vinaathari kubwa sana katika makuzi ya  kiakili ya mtoto”.

Tamko hili linaonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuona kwamba watoto wetu wanapata elimu katika mazingira salama na hivo kukuza uelewa wao, kuongeza ujasiri na kuwa na watoto wenye kujiamini na kuweza kuwa wabunifu kwa ustawi wa taifa letu. Tunaamini kuwa adhabu ni njia sahihi ya kumrekebisha mwanafunzi lakini hata hivo ni muhimu kuwa na adhabu zenye kujenga na ambazo hazina madhara kwa wanafunzi. Sisi kama wadau tumekua tukiomba serikali kuangalia adhabu mbadala ambazo hazina madhara kwa wanafunzi. Vilevile tumekuwa tukifuatilia ongezeko la adhabu zilizokithiri mashuleni haswa ndani ya mwaka 2018 ambazo zimepelekea vifo pamoja na ulemavu kwa baadhi ya wanafunzi.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inabainisha kwamba mamlaka ya nchi itaweka taratibu zinazofaa au zinazozingatia misingi kwamba ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha (Ibara ya 13 (6) (e))

Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inakataza mtu kumsababishia mtoto mateso, au aina nyingine ya ukatili au kumpa adhabu zisizo za kibinadamu au kumdhalilisha mtoto (kifungu cha 13 (1))

Sheria ya Elimu Sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002` Kifungu cha 61(1) (v) kinampa mamlaka Waziri wa Elimu kutunga kanuni  zitakazokidhi utekelezaji wa masuala ya sheria hiyo ya elimu. Kupitia mamlaka hiyo, moja ya kanuni zilizotungwa ni Kanuni ya elimu (Adhabu ya Viboko) (The Education (Corporal Punishment) Regulation G.N.294) ya mwaka 2002, zinazotoa mwongozo wa kutoa adhabu ya viboko, ikielezea wakati wa kutoa adhabu pamoja na

kiwango cha adhabu hiyo kwa mwanafunzi. Kanuni ya 3(1) inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule

ambalo litaishushia shule heshima. Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko 4 kwa tukio lolote.

Sheria inamtaka Mwalimu Mkuu wa shule husika kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo. Mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakuwa na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika.

Kanuni ya 5 inataka kila adhabu ya viboko inapotolewa kwa mwanafunzi kumbukumbu ya kutolewa kwa adhabu hiyo sharti iwekwe kwenye kitabu, na itaje jina la mwanafunzi, kosa alilolifanya, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu. Na kumbukumbu hizo lazima zisainiwe na Mkuu wa shule.

Hata hivyo kulingana na matukio mbalimbali nchini juu ya adhabu zilizokithiri kwa wanafunzi mpaka kupelekea vifo na ulemavu kwa baadhi ya wanafunzi ni dhahiri kwamba walimu hawazingatii kanuni hizi, hali hii imepelekea matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu kujitokeza mara kadhaa na kupelekea wanafunzi kushindwa kufurahia haki  ya elimu,  na kupelekea shule kutokua na mazingira salama kama ilivyotokea Bukoba.

Ili kufikia dhana ya elimu bora nchini Tanzania, na kuepuka adhabu zilizokithiri mashuleni, watetezi wa haki za watoto chini ya uratibu wa WiLDAF tunaiomba serikali kufutwa kabisa kwa adhabu ya viboka pamoja na adhabu nyingine zote zenye madhara kwa watoto na zenye kuwatweza. Aidha, tunaishauri serikali;

 1. Kuendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya walimu wanaotenda makosa ya jinai na ukatili wa aina nyingine kwa wanafunzi ili kuwa fundisho kwa wengine.
 2. Kupitia Wizara ya Elimu kuona uwezekano wa kurejea kanuni za utoaji adhabu shuleni. Kwa kutoa mafunzo ya mbadala wa adhabu za viboko kwa walimu. Licha ya uwepo wa kanuni hizo bado kumekua na ukiukwaji mkubwa wa kanuni zenyewe.  Hivyo ni wakati sasa serikali kuja na njia mbadala ya adhabu chanya ili kufanya mazingira ya shule pamoja na elimu kwa ujumla kuwa salama. Sisi kama wadau tuko tayari kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kuwa shuleni kunakuwa ni mahali salama kwa watoto kwa ajili ya kujifunza na hivyo kujenga taifa lenye ustawi na maendeleo ya nchi.
 3. Kuendelea kushirikiana na wadau kutoa  elimu juu ya Haki zao haswa katika maswala yanayohusu adhabu na kuwekwa mfumo mzuri wa kutoa taarifa pale haki zao zinapokiukwa. Hii hutokana  kwamba nyumbani wanakopeleka taarifa ndiko ambapo wazazi/walezi pia wanaona ni sahihi mtoto kupewa adhabu kali.

WiLDAF inaamini kwamba malezi mema na tabia nzuri inaweza kufundishwa bila kumuumiza mtoto kimwili na kiakili. Shule inapaswa kuwa sehemu salama kwa wanafunzi na kuwe na uhusiano mzuri kati ya mwalimu na mwanafunzi. Hii itasaidia elimu bora, kuheshimu haki za mtoto, pamoja na kupunguza wimbi la watoto wanaoacha shule kwa sababu ya adhabu zilizokithiri.

Tunakutakia kila la kheri katika shughuli zako za ujenzi wa taifa, barua hii imeandaliwa leo Tarehe 16/11/2018

Mratibu wa mradi.

Imeandaliwa na:

 1. Tanzania Gender Networking Program(TGNP)
 2. Tanzania Media Women Association(TAMWA)
 3. Tanzania Network of Ending Child Marriage
 4. Tanzania Child Forum Network
 5. Tanzania Domestic Workers Coalition(TDWC)
 6. Anti-Female Genital Mutilation Network (AFNET)
 7. Mwanza Children and Youth Network(MCYN)
 8. Tanzania Early Childhood Development Network(TACDEN)
 9. Zanzibar Women Lawyers Association (ZAFELA)
 10. Tanzania Association for children Advancement(ZACA)
 11. Tanzania Women Lawyers Association (TAWLA)
 12. Women Legal Aid Centre(WLAC)
 13. Women with Disability Network
 14. Mulika Tanzania
 15. Tanzania Youth Partnership country wide(TCYP)
 16. Haki za Wanawake (HAWA)
 17. Community Focus on Teenage and single mothers welfare(CFTSW)
 18. Vijana Assembly.
 19. People Development Forum (PDF).

 

This Post Has 0 Comments

Leave a Reply

Back To Top